Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, wanazuoni na wananchi wa Bangladesh, kwa kuandaa mkusanyiko na msururu wa watu katika mji wa Khulna, walitangaza mshikamano wao na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mtukufu Ayatollah Mkuu Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika kupinga njama za Marekani na ulimwengu wa Magharibi.
Katika mkusanyiko huo, kundi la wanazuoni, wanafunzi wa elimu za dini na tabaka mbalimbali ya wananchi walihudhuria, na kwa kupaza kauli mbiu, walionesha upinzani wao wa wazi dhidi ya sera za uvamizi za Marekani na nchi za Magharibi.
Katika mkusanyiko huo, Hujjatul-Islam Sayyid Ibrahim Khalil Razavi, Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia wa Bangladesh, akisisitiza msimamo wa kimsingi wa taasisi hiyo, alisema: Sisi daima tumesimama katika safu ya haki dhidi ya batili, na iwapo kuitetea haki kutahitaji kujitoa muhanga au hata kutoa maisha, hatutasita katika njia hiyo.
Akirejelea misimamo ya kihistoria ya Mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, aliongeza kuwa: Imam Khomeini (rehma za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) alikuwa amesisitiza kuwa mapinduzi haya yatasimama pamoja na waliodhulumiwa na dhidi ya madhalimu. Uvamizi wa Marekani dhidi ya Iran si tu ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu, bali pia unaweka usalama na uthabiti wa dunia nzima katika hatari kubwa.
Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia wa Bangladesh aliendelea kukosoa sera za kimataifa kwa kusema: Marekani, kwa kuleta migogoro ya bandia na kusukuma mbele sera mpya za ukoloni, inaendeleza utawala na udhibiti wake duniani. Hata hivyo, Umoja wa Mataifa na taasisi zinazodai kutetea haki za binadamu, licha ya vitendo hivi vya vurugu, zimekaa kimya.
Wahubiri wengine katika mkusanyiko huo, pia walilaani sera za uchochezi wa vita, vikwazo, kuzingirwa na vitisho, wakataka kusitishwa mara moja vitendo vya kibeberu, na wakasisitiza umuhimu wa kuheshimu matakwa ya mataifa, uhuru wa kitaifa wa nchi, na amani ya haki katika ngazi ya kimataifa.
Mkusanyiko huu wa maandamano ulifikia tamati kwa kusomwa kwa tamko la mwisho na kutangazwa mshikamano kamili na taifa na uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Maoni yako